Sina hakika kama kuna nia ya dhati kumkomboa msanii
FILAMU zimeibuka kuanzia
karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali
katika karne ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo
imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa
mengi.
Katika karne hii,
teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali vimeitangaza sana tasnia ya filamu kwa watu
wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea. Hata
hivyo, filamu nyingi zinazosambazwa kimataifa na kupenya soko la nchi nyingi ni
zile zinazozalishwa nchini Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya. Ukweli huu, pamoja na kutambua nguvu
ya filamu “inayoyumbisha mioyo na akili za watu” unaamsha wasiwasi kwa walio
wengi.