Picha zote kwa hisani ya Mwewe
NILIANDIKA wakati wa msiba
wa Kanumba kuwa umati wa watu waliojitokeza siku ya msiba wake ni ishara tosha
kuwa sekta ya filamu nchini ni kubwa na yenye nguvu kubwa lakini iliyotelekezwa
na serikali. Kama serikali itaamua kuzichukulia filamu kwa umakini mkubwa,
ikaandaa sera na kuunda chombo maalum kitakachoshughulikia filamu mfano wa kile
cha Afrika Kusini cha National Film and Video Foundation (NFVF), naamini kabisa
zinaweza kuwa chanzo kikubwa na muhimu sana katika kujenga taifa na zinaweza
kutumika kama jukwaa la kuchochea mijadala nchini kote.
Kupitia chombo chao cha
NFVF Afrika Kusini wanajivunia ‘hazina’ za sekta ya filamu ya nchi hiyo kama Tsotsi, iliyoshinda tuzo ya Academy mwaka 2006, Yesterday, filamu
nyingine iliyoshiriki tuzo za Oscar na iliyowahi kushinda katika tuzo
mbalimbali za kimataifa, na U Carmen E Khayalitsha, iliyoshinda tuzo ya Golden
Bear mwaka 2005 katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Berlin.
Muigizaji wa filamu ya Yesterday, Leleti Khumalo
Filamu ya Yesterday
Filamu ya Tsotsi iliyopata tuzo ya Oscar
Filamu hizi zimekuwa zikitia
chachu na hamasa kwa watengenezaji wa filamu wa Afrika Kusini kuwa wabunifu na
wenye kujali ubora. Vipi kuhusu sisi? Hivi serikali haidhani kuwa kuanzisha
chombo cha aina hii kutasaidia kutufanya tuwe na kazi nzuri ambazo siku moja
zinaweza kushinda tuzo katika matamasha makubwa na yanayoheshimika duniani?
Mbona hatujiulizi, sekta ya
filamu Tanzania inatengeneza sinema nyingi mno zinazoifanya kushika
nafasi ya tatu katika bara la Afrika, nyuma ya Nollywood (Nigeria na Ghana), lakini ni Afrika Kusini ambayo ina mafanikio
makubwa kwenye sekta ya filamu. Kwa nini hatujiulizi kuwa sinema nyingi za
bajeti kubwa na zenye mafanikio makubwa za kimataifa zimekuwa zikitengenezewa
Afrika Kusini.