Hans PR

Hans PR

Feb 25, 2011

Kwaheri Tabia wa Kidedea

 
Tabia alipokuwa akiigiza katika filamu ya Usiku wa Taabu
 Tabia alipokuwa akiigiza katika filamu ya Naomi

HAMISI KIBARI
Dar es Salaam

CHRIS Magori, mwandishi wa miongozo ya filamu (script), mtunzi na muongozaji (director), aliipenda hadithi niliyowahi kuiandika katika gazeti la Nipashe miaka ya nyuma ikiitwa 'Usiku wa Taabu'. Aliipenda hadithi hiyo kwa maana ya kuifanya filamu. Wakati huo, mwaka 2004, tasnia ya filamu ilikuwa inazidi kushika kasi nchini mwetu, lakini si kwa kiwango cha sasa.

Katika hadithi hiyo niliyoiandika kutokana na kisa cha kweli, mhusika mkuu ambaye ni mke wa mchungaji, alikuwa na tabia isiyoendana kabisa na hadhi yake. Kwa lugha nyingine alikuwa mhuni ambaye alidiriki kwenda gesti na wanaume hususan mumewe anapokuwa katika safari za kichungaji.

Katika tukio moja, mke huyo wa mchungaji aliwahi kwenda gesti na mmoja wa mume wa marafiki zake, tukio ambalo mwenye mume sambamba na mdogo wa mchungaji, yaani shemeji mtu waliandaa fumanizi.

Wakafuatilia hadi gesti alikoingia mwanamke huyo na hawara yake. Katika tukio hilo, mke wa mchungaji alilazimika kukimbia nje na mashuka ya gesti baada ya chumba alimokuwa na mume wa mtu kuvamiwa na shemejie pamoja na mke wa mwanaume aliyekuwa naye ambaye pia ni rafiki yake.

Katika tukio hilo, mchungaji ambaye alikuwa akimpenda sana mkewe, licha ya kusikia kwamba alikuwa anasumbuliwa na pepo wa ngono, alirejea na kumkuta mkewe akiwa hospitali, lakini kwa mshangao wa wengi akaamua kumsamehe akionesha pia uchamungu wa hali ya juu.

Baada ya Magori kuandika script na kuanza kusaka wasanii wa kucheza sinema hiyo, kazi kubwa ilikuwa ni kumpata mhusika mkuu, yaani atakayekuwa mke wa mchungaji.

Wasanii wengi waliopatikana, licha ya kuigopa nafasi hiyo kutokana na ukubwa wake, walionekana pia kutoitaka hasa kutokana na kuhusisha fumanizi la gesti na mhusika kukimbia nje na mashuka ya gesti. Kwa lugha nyingine wasanii waliopatikana waliinyanyapaa nafasi hiyo au naweza kusema tulio nao wengi ni aina ya wasanii wanaotaka kucheza sehemu wanazoonekana vizuri mbele ya jamii, na si sehemu ambazo wanadhalilika mbele ya macho ya Watazamaji. Tulio nao ni wasanii ambao wameshindwa kujua kwamba mtu anapocheza nafasi fulani kwenye filamu ama maigizo, anachofanya ni kuwakilisha yule mhusika aliye kwenye hadithi na si yeye binafsi. 
 
Baada ya wahusika waliokuwa wamepatikana kuiogopa nafasi hiyo, ndipo likatolewa wazo kwamba msanii anayeweza kuimudu, akavaa uhusika na kuicheza bila wasiwasi ni wa kutoka Kundi la Kidedea (sijui kama bado lipo), Dalila Peter Kisinda, aliyekuwa akijulikana zaidi kwa jina la usanii la Tabia.

Naam, msanii huyo alitafutwa na alipoambiwa kushiriki nafasi hiyo aliipokea kwa mikono miwili na kuifurahia.

Ni wakati wa mazoezi ya filamu hii ambapo mimi mwandika makala haya niliigiza kama mchungaji, yaani mumewe, nilipokutana na Tabia kwa mara ya kwanza. Hakuchelewa kunizoea na tukafanya vyema katika filamu hiyo kwa mujibu wa muongozaji, Magori.

Nilichogundua muda wote wa mazoezi yetu hadi kuitengeneza picha hiyo ni kwamba Tabia alikuwa na sifa zote za msanii mzuri. Alikuwa hachagui nafasi ya kucheza na alijitahidi sana kuvaa uhusika. Lakini kubwa kuliko yote nililoligundua kwake Tabia alikuwa mcheshi sana na mkarimu. Wengine ambao hawakupata bahati ya kuwa naye karibu wanaweza kudhani kwamba ucheshi wake ulikuwa ni wa kwenye sanaa tu, la hasha. Ni mcheshi kwa asili. Hata alipoamua kutega mazoezi Tabia alitumia pia usanii na utundu ili kufanikisha hilo.

Ninakumbuka siku moja alikuwa anataka atege mazoezi na alichokifanya, kwa sababu alikuwa na simu mbili, alijipigia, akahakikisha kwamba mlio ameusikia kila mtu akiwemo mwalimu Magori aliyekuwa akisimamia mazoezi kisha akapokea akijifanya anaongea na mtu anayemjulisha kwamba kuna tatizo la haraka nyumbani na anatakiwa.

Magori, aliamini ni kweli na kumruhusu Tabia kuondoka na huku nyuma aliacha kicheko baada ya wasanii wenzake kugundua kwamba Tabia alijipigia simu ile ili kupata ruhusa na kwamba alikuwa anaongea na simu ambayo haipo!

Hivi karibuni, baada ya kukaa mbali na masuala la filamu kwa muda mrefu kutokana na kubanwa na shughuli nyingi, niliamua tena kurejea kwenye filamu baada ya kuletewa hadithi nzuri iliyoandikwa na Winfrida Thomas.

Wakati mimi na Bishop John Hiluka tunajadili watu wa kushiriki kwenye filamu hiyo iitwayo Naomi, nilitoa pendekezo kwamba Tabia naye awemo na nikaamua kumtafuta. Kwanza nilikuwa ninashangaa kutomuona katika filamu nyingi zinazotoka. Nikawa ninajiuliza maswali, kwa nini inakuwa hivyo. Je, alikuwa ameachana na masuala ya filamu baada ya kuolewa?

Lakini mimi nilikuwa bado ninakumbuka uwezo wake wa kuigiza, ucheshi na ukarimu wake. Nilimtafuta na kumpata, akaniambia alikuwa yuko tayari kushiriki.

Sijaacha fani, bali majukumu tu yamenikabili, lakini nitajitaidi kutenga muda wangu nishiriki hiyo sinema,” alinijibu.

Naam, filamu hiyo tumeshaifanya na ingekuwa imeshatoka kitambo kama si kutofautiana kuhusu malipo na wasambazaji.

Katika hali ya kushangaza, wiki ambayo tumeanza mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaitoa filamu hiyo, ili watu wapate kumuona Tabia makali yake katika fani hii katika siku za karibuni, ndipo nikapata habari kwamba msanii huyo amefariki dunia.

Mimi ni mmoja wa watu ambao nimesikitika sana na mbaya zaidi nimepata habari huku Tabia niliyemheshimu sana katika fani akiwa keshazikwa na mbaya zaidi hakuwahi kuiona filamu hiyo aliyoshiriki kuicheza na inayotarajiwa kutoka punde.

Ni masikitiko kwangu kwani, baada ya kuamua kurudi kwenye filamu na michezo ya kuigiza baada ya kukaa nje kwa kipindi kirefu kidogo, nilimtegemea Tabia kuendelea kuwa mmoja wa washiriki muhimu katika filamu zinazotokana na hadithi zangu.

Lakini ndivyo mapenzi ya Mungu yalivyo. Yeye amempenda zaidi. Ninamuomba Mwenyezi Mungu amuondolee madhambi yake na kumlaza mahala pema kwani yeye ametangulia tu.

Ina Lillahi, wa ina ilaihi Rajiuun.

Feb 23, 2011

Utamaduni wa Mtanzania ni upi, na unahusishwaje na filamu zetu? KULIKONI FEB 25, 2011

 Filamu iliyozua utata ya Shoga

 Filamu ya Off Side

KWA kweli suala la mila na utamaduni wa Mtanzania linatatiza sana. Tunaposema utamaduni na mila za Watanzania hasa tunamaanisha nini kwa Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake? Huu utamaduni na mila za Watanzania ni upi hasa?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo kila mtetezi wa mila na utamaduni ndani ya jamii za Kitanzania anapaswa kuyajibu. Vinginevyo tutakuwa tukiimba wimbo tusioujua maana yake, na hii haitatusaidia kufikia malengo tunayoyapigania.

Siku za hivi karibuni kulifanyika uzinduzi wa filamu ya Shoga ambayo kabla haijaingia sokoni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilibidi iingilie kati kwa kuiagiza Kampuni ya kutengeneza filamu ya Al-Riyamy Production Company kuiwasilisha filamu hiyo kwa Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi.
 
Tukio hilo limefuatia baada ya watu wengi wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari kuilalamikia filamu hiyo hata kabla hawajaiona wakidai kuwa inapotosha maadili na haiakisi utamaduni wa Watanzania. Naomba niweke wazi, makala yangu haikusudii kuendeleza mjadala kuhusu filamu hiyo bali ieleweke kuwa sakata hilo ndilo lililonifanya kuibua mada kuhusu utamaduni wa Watanzania.

Utamaduni ni neno lenye asili ya Kilatini “Cultura” ambalo lina usuli wake katika neno colere, linalomaanisha “kulima”. Neno hili lina fafanuzi nyingi. Kwa mfano, mwaka 1952, Alfred Kroeber na Clyde Kluckhohn walikusanya orodha ya vielelezo 164 vya neno “utamaduni” katika kazi yao: Culture: a Critical Review of Concepts and Definitions.

Hata hivyo, neno “utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:
-Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vilevile hujulikana kama utamaduni wa juu
-Mkusanyiko wa maarifa ya kibinadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kiishara
-Ni jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi fulani.

Dhana hii ilipoibuka kwanza katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa barani Ulaya, ilimaanisha mchakato wa kulima au kuboresha kilimo au kilimo cha mboga. Katika karne ya kumi na tisa dhana hii ilimaanisha kuboreshwa kwa mja kupitia elimu na hali kadhalika ilimaanisha kutekelezwa kwa maazimio ya kitaifa au maadili.

Katikati mwa karne ya kumi na tisa, wanasayansi wengine walitumia dhana ya utamaduni kurejelea uwezo wa kiubia wa binadamu.

Katika karne ya ishirini, “utamaduni” ilijitokeza kama dhana ya kimsingi katika somo la Anthropolojia. “Utamaduni” ulihusisha mambo yote yaliyomhusu binadamu ambayo hayakufungamana na matokeo ya kimaumbile. Dhana ya utamaduni katika Anthropolojia ya Kimarekani ilikuwa na maana mbili: (1) Uwezo wa kibinadamu wa kuainisha na kuwasilisha tajiriba za kibinadamu kiishara na kutenda mambo kiubunifu; na (2) Namna mbalimbali watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni huainisha na kuwasilisha tajiriba zao za maisha na kutenda mambo kiubunifu.

Kufuatia vita vya pili vya dunia, dhana hii ilipata umaarufu ingawa na fafanuzi tofauti tofauti katika taaluma kama vile sosholojia, Mafunzo ya utamaduni, saikolojia ya mipangilio na mafunzo ya usimamizi.

Leo hii tukiwa tunaelekea miaka 50 ya Uhuru wetu hapo Disemba 9, jamii ya Kitanzania inaonekana kupoteza mila na tamaduni zake kila kukicha.

Utata unaojitokeza kuhusu neno utamaduni wa Mtanzania, binafsi nadhani kuwa utamaduni tunaoweza kuuita wa Watanzania unamaanisha lugha ya Kiswahili, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi, ujenzi wa nyumba na tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika).

Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo kikuu cha ndani cha jamii yetu. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.

Ikumbukwe kuwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962. Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.


Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.

Pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwenye jamii yetu lakini bado sera ya utamaduni hapa nchini imekuwa haipewi nafasi katika serikali hii tangu ilipoanzishwa wizara inayoshughulikia masuala ya sanaa. Tangu mwaka 1962 shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi.

Ingawa mimi si mtu wa imani ya kiroho lakini naamini kuwa hali ya mtu kujitenga na tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi tuziishizo. Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu, upendo na kadhalika.

Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumba sana vijana ambao bila kujua huwa tunajikuta katika utamaduni hasi unaotusukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na kukosekana kwa tamaduni.


Hii inajionesha hasa katika sanaa zetu na hasa filamu tunazoziandaa ambazo nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetupelekea kukosa kabisa vipaumbele katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.

Filamu zisizo na maadili si zile zenye majina yanayoashiria mmomonyoko wa maadili tu kama ilivyo kwa filamu ya Shoga, ambayo mbali na jina lake kama utabahatika kuitazama kwa kweli utakubaliana nami kuwa mambo yanayolalamikia na watu wala hayajaoneshwa kabisa, iko tofauti kabisa na filamu zenye majina mazuri yasiyoashiria mmomonyoko wa maadili lakini maudhui yake hukosa kabisa maadili.

Katika hili watu wameingia katika mkumbo wa wengi kuhukumu jina la kitabu zaidi ya vilivyoko ndani. Sijui hapa tunalalamikia jina au maudhui yaliyomo ndani ya sinema? Na kama ni maudhui, je hizi zenye majina mazuri lakini hadithi zake zinakosa maadili zinaziongeleaje? Mbona Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo haijawahi kuagiza zipelekwe Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi?
 
Ninachoamini ni kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, jambo hili linaonesha umuhimu wa utamaduni si kitu kilichoibuka tu.

Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.


Sanaa yetu ya filamu imesahaulika kabisa, na tumepokea ile ya nje tena kwa fujo, hali hii imesababisha Watanzania kuwa wafuatiliaji na waigaji wa filamu za nje badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili filamu zetu ziende na matakwa ya dunia kwa kuziboresha.

Sasa ni wakati muafaka wa kujaribu kufikiria na kuchambua kila tunapoiga mambo ya kigeni iwapo yana mchango wowote katika makuzi ya tamaduni zetu au yanakuwa chanzo cha kuziangamiza. Hatuna budi kuelewa kwamba kuanguka kwa tamaduni ni anguko letu pia.


Tunapaswa kuiga hekima na busara za wenzetu waliondelea na kuacha yale yasiyofaa ambayo yanatupotosha. Ni wakati sasa wa kuyatenda yale tunayoyahubiri na kuacha propaganda zisizotusaidia kuboresha kazi zetu.

Alamsiki

Feb 22, 2011

Wasanii watakiwa kuacha kulewa sifa

Sehemu ya mji wa Morogoro

Husna Posh (Dotnata), mmoja wa wasanii wenye mafaniko makubwa

Na Ashton Balaigwa
Morogoro

Wasanii nchini wametakiwa kuacha kulewa sifa mara baada ya kupata mafanikio na badala yake watumie vipaji walivyonavyo kuelimisha kwa kutumia njia zitakazoisaidia jamii kutambua mahala tulipo na tunakoelekea.

Wito huo umetolewa na mwanasheria wa Kituo cha Wasaidizi wa Sheria kwa Wanawake na Watoto cha mjini Morogoro, Aman Mwaipaja, wakati akizungumza na wasanii chipukizi wa maigizo wa Kikundi cha Mikano Arts Group.

Mwaipaja aliwataka wasanii hao kujituma ili waweze kupata mafanikio kama wasanii wengine wakubwa na kuacha tabia ya majigambo.

Aliwataka wasanii hao kuchekesha kwa kutumia kipaji walichopewa na Mungu katika kuelimisha jamii kama walivyofanikiwa wasanii wengine wa kuchekesha. Aidha aliwataka wasanii hao kutunga maigizo yanayotoa elimu kuhusiana na gonjwa la Ukimwi kwani bado kuna baadhi yao hawana uelewa wa kutosha licha ya kuwa elimu hiyo inatolewa kaatika maeneo mengi.

SOURCE: NIPASHE

Feb 21, 2011

Serikali yasitisha usambazaji wa filamu ya Shoga


 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 Poster ya filamu ya Shoga

Hisani Muya (Tino), mtunzi na mhusika mkuu wa filamu ya Shoga

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeiagiza Kampuni ya kutengeneza filamu ya 'Al-Riyamy Production Company' kuwasilisha Filamu ya 'Shoga' kwa Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi.

Aidha Kampuni hiyo pia imeagizwa kutoisambaza Filamu ya 'Shoga' na kusitisha hatua nyingine yoyote kuhusiana na filamu hiyo hadi hapo Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu itakapojiridhisha kuwa filamu hiyo inakidhi kuonyeshwa hadharani kama ilivyoainshwa katika Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwani Namba 4 ya mwaka 1976.

Kampuni hiyo inatakiwa kuwasilisha kanda hiyo kabla ya tarehe 17 februari, 2011.Kwa mujibu wa Sheria hiyo hairuhusiwi kutengeneza filamu bila kupata kibali cha kutengeneza filamu.
Aidha kifungu cha 4 (1) inaelekezwa bayana kuwa kila anayetengeneza filamu anatakiwa kuwasilisha maombi kwa maandishi kwa Waziri chini ya Sheria hii yakiambatana na mswaada na maelezo ya filamu inayotarajiwa kutengenezwa.

Pamoja na mambo mengine katika kifungu cha 14 (2) Sheria inaipa Bodi ya Filamu mamlaka ya kukagua filamu, picha ya matangazo au maelezo yake kwa makusudi ya kuamua kuonyesha na ikiwa rushusu itatolewa maonyesho yawe kwa namna gani.

Katika Sheria hiyo kifungu cha 15 (1) kinapiga marufuku kwa mtu yoyote kuongoza,kusaidia , kuruhusu au kushiriki katika maonyesho ya filamu bila kuwa na kibali cha Bodi.
Sheria hii ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa waraka Namba 22 wa mwaka 1974.

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Tarehe 14 februari, 2011.

ARTERIAL Network: Mtandao wa wasanii uliozinduliwa Tanzania

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo wa Zanzibar, 
Abdillah Jihadi aliyekuwa mgeni rasmi siku ya uzindua 
wa Mtandao wa ARTERIAL Tanzania. Wengine ni 
Mwenyekiti mpya wa Mtandao huo nchini, Laurian Kipeja (kati) 
na kushoto ni mwakilishi wa Mtandao huo kwa Afrika, 
Telesphore Mbabizo.

Picha ya pamoja na Mgeni Rasmi.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa Mtandao wa ARTERIAL Tanzania

Mtandao wa wasanii Barani Afrika unaojulikana kwa jina la ARTERIAL Network, umezindua tawi lake nchini Tanzania na tayari umepata viongozi watakauongoza kwa kipindi cha miaka mwili.

Uzinduzi wa mtandao huo ulifanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mh. Abdillahi Jihadi, katika hoteli ya Zanzibar Grand Palace.

Mmoja wa viongozi waliochaguliwa kuuongoza mtandao huo kwa kipindi cha miaka miwili ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habri za Sanaa na Utamaduni Tanzania (CAJA), Hassan Bumbuli, aliyechaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa mtandao huo, huku aliyekuwa mratibu wa kamati ya muda ya mtandao huo Tanzania, Laurian Kipeja akichaguliwa kuwa Mwenyekiti.

Wengine ni Ali Bakari aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti, na wajumbe watano wanaowakilisha sekta mbalimbali za sanaa ikiwemo muziki, sanaa za maonesho, sanaa za ufundi, filamu na sekta ya habari.

Wajumbe waliochaguliwa na nafasi zao kwenye mabano ni pamoja na Sauda Simba Kilumanga (Muziki), Godfrey Lebejo Mngereza (sanaa za maonesho), Sabrina Othman (filamu), sharifa Juma (Sanaa za Ufundi) na Sofia Ngalapi (Habari).

Feb 17, 2011

Shirikisho la Filamu Tanzania laitaka serikali kuwekeza kwenye filamuShirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) limeitaka serikali kuwekeza katika kazi za sanaa ya muziki na filamu ili kukuza pato la taifa.

Hayo yalisemwa na Rais wa sirikisho hilo, Simon Mwakifwamba, katika uzinduzi rasmi wa shirikisho hilo ulioambatana na Tamasha la Filamu za Kitanzania “The Mwalimu Nyerere Film Festival” lililoanza Februari 14 katika viwanja vya Leadres Club vilivyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Tunaiomba serikali iliangalie hili, kwani sekta ya sanaa ina mapato makubwa sana ambayo yanaweza kuiendesha nchi iwapo serikali italizingatia hili. Si hivyo tu bali itaweza kutukomboa wasanii kwa namna moja ama nyingine kutokana na wizi ambao umeeenea hivi sasa,” alisema.

Alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapaswa kuzingatia na kuhakikisha mapato yatokanayo na sanaa ya muziki na filamu yanapatikana, kuliko kuwaachia wachache ambao wananeemeka kwa kuwafaya wasanii kurudi nyuma huku serikali ikikosa mapato.

Alisema kwa sasa shirikisho hilo lipo katika wakati mgumu na kuiomba serikali iwasaidie hasa kwa vile wanategemea kufanya tamasha kubwa la filamu baadaye Septemba mwaka huu.

Source: Mwananchi

Wahujumu wa kazi za Wasanii waanikwa mkoani Pwani

 Kazi feki za sanaa zikiwa tayari kwa kuuzwa

Kazi feki zikitayarishwa kuchomwa huko China

Kundi la watu ambao wamekuwa wakihujumu kazi za wasanii mbalimbali nchini limebainika mkoani Pwani.

Uchunguzi uliofanywa kwa muda mrefu katika magulio kadhaa ya mkoa wa Pwani umebaini kuwapo kwa kundi kubwa la wafanyabiashara wanaouza kazi za Wasanii mbalimbali zilizodurufiwa (duplicated) kwa bei ya chini na kusababisha wasanii kutofaidika na kazi zao.

Uchunguzi huo wa muda mrefu katika wilaya za Bagamoyo, Kisarawe, Rufiji na Mkuranga umebaini kuwapo kwa wauzaji hao wa kazi za wasanii ambao wamekuwa wakidurufu na kuziuza kazi hizo kwa bei ya chini ya shilingi 1000.

Miongoni mwa kazi ambazo zimekuwa zinaongoza kwa kuuzwa kwa wingi katika magulio hayo ni kazi za muziki wa injili za Rose Mhando na video za filamu za wasanii ambazo nyingi zimechezwa na wasanii nguli; Vincent Kigosi "Ray", Steven Kanumba na Blandina Chagula "Johari".

Source: Mtanzania

Waziri Nchimbi, ni lini sekta ya filamu itakuwa rasmi? KULIKONI FEB 18, 2011

 Waziri wa Habari, Maendeleo ya Vijana, 
Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi

KWANZA kabisa napenda nikupongeze kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Habari Vijana na Michezo, nikitumaini kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuona unafaa zaidi kuiongoza wizara hii nyeti inayohusu mustakabali wa utamaduni wa Watanzania.

Nakubaliana na wanaosema kuwa uteuzi wako kuiongoza wizara hii umewapa wanahabari na wasanii tumaini jipya kwa sababu tangu nchi yetu ipate uhuru miaka 49 iliyopita, wizara hiyo ilimpata waziri mmoja tu, Marehemu Ahmed Hassan Diria, aliyesimamia kwa dhati maendeleo ya wanahabari/ wasanii na ustawi wa tasnia nzima. 
 
Nakuhakikishia kuwa wizara unayoiongoza imesheheni utajiri mkubwa sana wa utamaduni na uchumi kupitia filamu za Kibongo. Tatizo ni kwamba hadi sasa tasnia ya filamu bado haijawa rasmi.

Sekta ya filamu na burudani kwa sasa inakua kwa kasi, hivyo, nguvu kubwa lazima iwekezwe ili kuhakikisha kuwa sekta hii inakuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato miongoni mwa Watanzania ikiwa ni pamoja na kulitambulisha taifa katika ngazi mbalimbali za kimataifa.

Waziri, sina hakika kama wizara yako inaielewa nguvu ya soko letu na umuhimu wa utamaduni na uchumi kupitia filamu za Kibongo, na iwapo itasimamia vyema basi tasnia hii itasaidia kupanuka kwa ajira hapa nchini.

Mbali na hilo, nakusihi ujaribu kuangalia suala zima la wizi wa kazi za wasanii kwa kuzitazama upya sheria dhaifu za hakimiliki, na kutusaidia kupigana na wezi hawa kwa kushiriki kutunga sheria kali au kutoa hoja kuhusu tatizo hili ambalo kwa sasa limekuwa sugu.

Vilevile nakuomba ujaribu kuangalia uwezekano wa kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuwawezesha watengenezaji wa filamu, ili kuondoa mfumo uliopo kwa baadhi ya wafanyabiashara wachache kushikilia biashara hiyo, wapo wanaodhani tuwe na Tume ya Filamu (
Tanzania Film Commission) itakayotoa misaada kwa watengenezaji wa filamu ikiwa na jukumu la kuongeza ujuzi katika uandishi wa miswada na utayarishaji wa filamu.

Nimewahi kumshauri Rais ajaribu kuwaagiza watendaji wake kuutazama mfumo unaotumiwa nchini Afrika Kusini kupitia chombo chao kinachojulikana kama National Film & Video Foundation (VFVF), na uwezekano wa kuwa na chombo cha aina hii kwa maendeleo ya tasnia yetu.

Katika kufanikisha jambo hili ni lazima kiundwe chombo kitakachoongozwa na Baraza linalojumuisha wanataaluma wanaoheshimika sana katika filamu na utaalamu wa aina mbalimbali katika sekta ya filamu na televisheni, wasanii waliobobea na wenye uelewa mkubwa na wasambazaji ili kuweza kuwakilisha vyema mbinu na mikakati sahihi kwa niaba ya serikali.
Chombo hiki lazima kijue tatizo la msingi linalowakabili wahusika, na kiangalie maslahi kwa pande zote zinazohusika na biashara hii. 
 
Chombo hiki kiwe chombo cha kisheria kitakachopewa mamlaka na bunge kuongoza maendeleo ya sekta ya filamu na video hapa nchini. Visheni ya chombo hiki iwe kuhakikisha kunakuwepo ubora wa filamu katika tasnia ya filamu na video Tanzania zinazowakilisha taifa, kibiashara na kuhamasisha maendeleo.

Kama ilivyo kwa Afrika Kusini, chombo hiki kiundwe ili kusaidia kujenga mazingira ambayo yanaendelea na kudumisha sekta ya filamu na video, ndani ya nchi na kimataifa.

Waziri, najua unajua kuwa tasnia ya filamu lazima iongozwe na maadili, vivyo hivyo chombo hiki kiwe na maadili muhimu ya kujenga mazingira kwa ajili ya Watanzania wa kawaida, kubeba ushawishi katika kazi zao wenyewe, na hivyo kuimarisha demokrasia na kujenga mafanikio.

Chombo hiki kiwe na malengo makuu kumi yanayotokana na mpango wa biashara yake kama vile mamlaka yake kutoka kwa serikali:
-Kuendeleza uhusiano bora kati ya serikali, sekta ya filamu na taasisi za udhibiti.
-Kupata fedha kwa njia ya fedha za umma, uwekezaji binafsi, bahati nasibu na njia nyingine.
-Kuchochea na kuendeleza maendeleo ya ujuzi, elimu ya filamu na mafunzo.
-Kufuatilia, kupima na kupanga mikakati ya kitaifa kwa ajili ya tasnia, na kutoa ushauri kwa serikali juu ya sera zifaazo.
-Kuendeleza bidhaa za ndani na uzalishaji.
-Kuwaendeleza watazamaji wa filamu na televisheni wa Tanzania ili kuthamini mchango wao kwa kununua kazi zinazozalishwa ndani ya nchi.
-Kukuza mauzo ya filamu nje ya nchi, na kuvutia uwekezaji na uzalishaji wa kimataifa.
-Kurekebisha usawa katika sekta ya filamu na kuendeleza biashara ndogondogo na za kati kwa ajili ya ukuaji wa ufanisi katika sekta hii.
-Kusaidia kutafakari utamaduni na lugha ya Watanzania kwa watazamaji wa ndani na wa kimataifa.
-Kutoa fursa na fedha kwa ajili ya maendeleo ya filamu, uzalishaji, maonesho na mafunzo.

Lakini huwa napata shida kidogo kutokana na ukweli kwamba watengenezaji wa filamu waliopo kwenye soko letu wamekosa mfumo mzuri wa kuwawezesha kupata msaada wa mitaji kwa kazi zao. Hata hivyo, kwa mtazamo wangu, nakushauri ujaribu kuangalia kwa makini jinsi watengenezaji filamu wanavyoandaa miundo ya kihazina (funding structure) katika kampuni zao kabla haujaelekeza nguvu zako katika kusaidia sekta hii.

Waziri, najua unaelewa fika kuwa sekta ya filamu ni nguvukazi kubwa na hivyo ni moja ya sekta muhimu, ikiwa itaungwa mkono na serikali, inaweza kuchangia sana upatikanaji wa ajira. Wizara yako inapaswa kuelekeza nguvu nyingi katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wasanii na watengeneza filamu. 
 
Kama nilivyowahi kumwandikia rais, suala la kutafuta gharama za mafunzo kwa watengeneza filamu linapaswa kuwa jambo la kwanza kabisa kwa wizara yako katika kuutambua mchango wa sekta ya filamu. 
 
Elimu na mafunzo ni ufunguo muhimu sana kwa ukuaji na uendelevu wa sekta ya filamu na video, na hata mafanikio ya tasnia hii hasa kama sekta itafaidika kutokana na mahitaji ya kimataifa ya burudani ya filamu ambayo inakua sambamba na teknolojia ya digitali inayofanya kuongezeka kwa idadi na aina ya vyombo vya utoaji wa filamu. Tasnia ya filamu, kwa asili yake, inaendeshwa na mambo makuu mawili; vipaji na ujuzi. 
 
Waziri, lengo la msingi la chombo ninachopendekeza liwe kutoa mkakati wa kitaifa na uongozi wa maendeleo ya kimitaji katika Sekta ya Filamu na Video ndani ya mfumo kwa niaba ya serikali na kutangaza sera ya kazi kwa njia ya Mkakati wa Taifa wa Stadi na Maendeleo, na hivyo kuchangia kuboresha uzalishaji na ushindani wa sekta, na kukabiliana na changamoto za maendeleo ya kijamii na kuondokana na umaskini. 
 
Pia chombo hiki kiweze kutoa na kuhimiza utoaji wa nafasi kwa ajili ya watu, hasa wanaotoka katika jamii yenye matatizo kushirikishwa katika sekta ya filamu na video.

Kuwepo uthamini katika kupeana mrejesho kutoka kwa mtunzi wa wazo kupitia awamu zote za uzalishaji, usambazaji, utoaji na njia ambayo watazamaji watapokea na mwitikio wa bidhaa (Filamu, vipindi vya televisheni, Video, nk.) ambayo kwa upande wake, hujazwa katika hadithi iliyoandikwa na utafiti na huishia kwenye muongozo (scripts) au majarida ya filamu na makala (documentaries). 
 
Chombo hiki kiweze kutoa takwimu za kina na za kuaminika, utafiti unaoendelea juu ya mahitaji ya ujuzi uliopo, elimu na utoaji wa mafunzo pamoja na kubaini mapungufu. Kufanya uratibu wa pamoja na mbinu ya kutoa elimu na mafunzo kulingana na mahitaji ya tasnia.

Pia kiweze kusimamia elimu ya filamu na mafunzo bora ya uhakika, manunuzi kutoka sekta ya filamu kwa ajili ya Mkakati wa Taifa wa Stadi na Maendeleo na mifumo yake ya kutekeleza.
Kiwe na mkakati madhubuti wa mawasiliano kwa ajili ya elimu na mafunzo ya filamu, mkakati imara wa ushirikiano na wadau wa umma na sekta binafsi kutoa uratibu na ufanisi wa kifedha kwa ajili ya elimu ya filamu na mafunzo.

Pia uwepo uratibu na usimamizi wa mgao wa ruzuku kwa ajili ya maendeleo ya ujuzi kuendana na mahitaji ya ujuzi na malengo ya chombo hiki ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma ya elimu ya filamu na mafunzo.

Chombo hiki kizingatie kusaidia uzalishaji wa filamu na makala (documentaries) ama kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu au ruzuku. Chombo kichukulie utoaji pesa za uzalishaji kama uwekezaji na kitafidia matumizi yake wakati wa utoaji wa bidhaa iliyokamilika kupitia usambazaji wa ndani wa kibiashara na njia ya maonesho. Pia chombo hiki kitaamua kwa hiari yake ni aina gani ya msaada kiutoe. 
 
Naamini kuwa mafanikio ya filamu yoyote iliyokamilika au uzalishaji wa video hutegemea masoko na kukuza ubunifu. Chombo hiki kitoe mikopo ipasavyo kwa ajili ya matangazo na masoko ili kuhakikisha uzalishaji wa filamu na video za Tanzania kwa watazamaji wa ndani na wa kimataifa unakua.

Mwisho, chombo hiki kitoe msaada kwa watengeneza filamu na wasambazaji kwa ajili ya kukuza ufanisi wa bidhaa zao katika masoko ya filamu na matamasha.
Naomba kuwasilisha...

Feb 9, 2011

Kutoka Mahoka, Pwagu na Pwaguzi hadi maigizo yenye mizaha! KULIKONI, FEB 11, 2011

Marehemu Mzee Pwagu, mmoja wa wachekeshaji 
waliojizolea umaaruf mkubwa nchini

Said Ngamba (Mzee Small), mchekeshaji 
wa kwanza Tanzania kuigiza kwenye Televisheni

Charlie Chaplin, mchekeshaji maarufu wa enzi za 'silent film'

Mr Bean, mchekeshaji maaruf wa Uingereza

WIKI iliyopita nilimkuta binti yangu wa miaka 6, Magdalena, akiwa na mama yake wameketi sebuleni wakiangalia katuni za Tom & Jerry, nilichukua rimoti na kuwabadilishia nikiweka kipindi cha Komedi kinachorushwa na moja ya vituo vyetu vya televisheni, kipindi kilichokuwa gumzo sana siku za nyuma na kilipendwa na watu wa rika zote.

Niliweka kipindi hicho nikijua wao ni wafuatiliaji wakubwa, kuna wakati tulikuwa tukigombana kwa kuwa walitaka kuangalia komedi hata pale nilipokuwa nikifuatilia habari muhimu kwenye vituo vingine.

Niliweka komedi nikiamini kwamba hawakujua kama kipindi wakipendacho kilikuwa hewani, kumbe nilikosea kwani binti yangu alinijia juu akitaka niondoe kipindi hicho huku akiungwa mkono na mama yake, hapa nanukuu alichosema; “Ondoa mimi sitaki hiyo, kwanza watu wenyewe siku hizi hata siwaelewi,” mwisho wa kunukuu.

Comedy ni neno la Kiingereza lenye asili ya Ugiriki likimaanisha futuhi au ucheshi kwa Kiswahili, ni vichekesho (humorous) vyenye lengo la kufurahisha, kufundisha na kuburudisha watazamaji, hasa katika televisheni, filamu, na kwenye majukwaa ya sanaa. Inasemwa kwamba unapocheka ndivyo maisha yanavyokuwa bora zaidi!

Ucheshi ni kama mwanga unaouangazia moyo, ni igizo lililobuniwa ili kuchekesha, kuburudisha, na kumfanya mtu astarehe. Muundo wa ucheshi ni kuzidisha hali ya mambo ili kuleta uchekeshaji, kwa kutumia lugha, matendo, na hata wahusika wenyewe.

Ucheshi mara nyingi huhoji na kufuatilia kwa makini yalipo mapungufu, makosa au hitilafu, na vitu vinavyokatisha tamaa ya maisha, na kuleta uchangamfu na wasaa mdogo wa kufurahia maisha ya kila siku.

Tasnia ya filamu hasa katika ucheshi imekuwa inasonga mbele na kuzidi kujizolea umaarufu siku hizi, vijana wengi wanajitokeza kuingia kwenye sanaa ya uigizaji wa vichekesho. Navutiwa sana na ari ya sanaa ya vijana wa Kitanzania pamoja na kuwepo mapungufu.

Enzi zile nikiwa mdogo, kabla sijaanza darasa la kwanza na hata baada ya kuingia shule ya msingi tulizowea kusikiliza vipindi vya Mahoka na Pwagu na Pwaguzi, vikirushwa na Redio Tanzania, hakuna shaka hawa jamaa walikuwa vinara wa vichekesho kwa jinsi walivyoweza kupangilia vituko vyao japo tulisikia sauti tu bila kuwaona.

Na kwa waliokwenda kwenye kumbi mbalimbali hasa hapa Dar es Salaam na miji mikubwa walikutana na vikundi vya sanaa kama Kibisa, Muungano, Mandela, Bima nk. na hawakukosa kufurahia vichekesho vya kina King Majuto, Braco Minyugu, Bartholomeo Milulu na wengineo.
Ukija kwenye magazeti pia kulikuwa na vikaragosi maarufu vya Chakubanga na Polo, na baadaye Kingo ambaye bado yupo hadi sasa. Pia jarida la Sani na vikaragosi waliodumu hadi sasa kama Komredi Kipepe, Madenge, Dk. Love Pimbi, Sokomoko, Profesa Ndumilakuwili, Lodi Lofa nk.

Kwa kawaida wachekeshaji (Comedians) ni wasanii ambao wana umuhimu wa aina yake katika jamii. Hawa ndio hufanya wakati mwingi watu tusahau uchungu wa maisha kwa jinsi ambavyo wanatuvunja mbavu tukiwasikiliza redioni, kuwaona kwenye televisheni au hata kukutana nao mitaani. Isitoshe wasanii hawa, kwa kupitia michezo au vichekesho vyao, hutoa mafunzo mazuri sana kwa kijamii.

Kwa bahati mbaya sana, nchini Tanzania bado hakuna mifumo mizuri kwa ajili ya wasanii kama hawa kufaidi vizuri jasho litokanalo na kazi zao. Wengi wao wanakuwa na hali ya kimaisha isiyolingana na vipaji walivyonavyo.

Baada ya kuanzishwa vituo vya televisheni hapa nchini mwaka 1994, aliibuka Mzee Small, baadaye Mzee Majuto na wenzake na hata Onyango na wenzake, ambao nakiri kuwa walituburudisha sana.

Kisha wakaja Max na Zembwela na 'Mizengwe' yao na kutoa burudani kulingana na wakati. Baada ya kifo cha Max, Zembwela na Mizengwe walianza kuchuja taratibu, ndipo wakaibuka Ze Comedy (EATV) ambao waliuteka umma wa Watanzania kwa vichekesho na staili ya taarifa ya habari.

Hivi sasa kumeibuka wasanii na vikundi vingi wanaoigiza kile kinachoitwa vichekesho (comedy) kwenye televisheni na filamu ambazo zinatoka kila kukicha. Lakini, ukweli ni kwamba wanachoigiza sidhani kama kinapaswa kuitwa vichekesho bali maigizo yenye mizaha. 
 
Msomaji mmoja alinitumia ujumbe wiki chache zilizopita akiniuliza kama maigizo ya mizaha siku hizi ni comedy? Na kama ni hivyo na ucheshi utaitwaje?

Komedi kwa kawaida imegawanyika katika mifumo ya aina kuu mbili: comedian-led (wachekeshaji), kwa kutuletea kichekesho kilichopangiliwa vizuri, utani au michoro, na situation-comedies au kwa kifupi “sit-com” ambayo huelezea stori/ kisa kilichomo ndani ya hadithi inayosimuliwa.

Situational comedy ni aina ambayo kisa husimuliwa na kinachekesha wakati mwingine bila kuanza na stori fulani kuhusu tukio au jambo.

Vipengele vyote vya ucheshi vinaweza kuonekana kwa pamoja na/ au kuingiliana. Pia kuna mfumo wa ucheshi unaojulikana kama 'Comedy hybrids' ambapo huenda pamoja na aina nyingine: musical-comedy (ucheshi kwa njia ya muziki), horror-comedy (ya kutisha), na comedy-thriller (ya kusisimua).

Pia kuna ucheshi wa papo kwa papo jukwaani (stand-up comedy), aina hii ya ucheshi ambayo Wakenya wamefanikiwa sana, mfano kundi la Ridiculous lililojulikana zaidi kama “Red Corna ambalo Ze Comedy waliiga ucheshi wa papo kwa papo lakini wakashindwa kabla hawajarukia kuigiza taarifa ya habari ambayo pia wameiga kutoka Red Corna ya Kenya.

Niliwahi kushuhudia jinsi Ze Comedy walivyokuwa wanahangaika kuchekesha papo kwa papo pale kwenye ukumbi wa Starlight! Aina hii ya ucheshi wa papo kwa papo inahitaji uelewa mkubwa sana wa jambo unalotaka kuliigiza ili lichekeshe, kwani kichekesho kinategemeana sana na tukio la papo kwa papo au lililotokea!

Hii ni kwa sababu sisi Waaafrika kwa sehemu kubwa hutumia ishara, mifano katika hadithi na matukio ya kuchekesha. Ucheshi kwa kawaida huwa na mwisho wenye kufurahisha, ingawa wakati mwingine unaweza kuegemea mambo yanayosisimua au mabaya.

Sikatai, hapa Tanzania wapo baadhi ya wachekeshaji wazuri sana lakini wamekosa mwongozo mzuri wa kuwafanikishia kazi zao. 

Wachekeshaji wetu wanapaswa kuongeza wigo wa ubunifu na kujifunza zaidi kama wanataka kuendelea kutusisimua, aidha wanapaswa kufuatilia vichekesho vya wenzetu ikiwa ni pamoja na kununua kazi hizo, wawashirikishe wengine, wabadili mfumo, watafute maoni, watumie lugha sanifu, wazame ndani ya akili za wateja wao kujua mahitaji yao na wasome alama za nyakati.

Kutokana na haya nakubaliana na binti yangu aliyesema kuwa siku hizi hawaeleweki, kwani sioni kama kuna ubunifu wa kuchekesha zaidi ya kufanya mizaha na kuwakashifu watu wengine. Ni vichekesho gani hivi hata kufikia hatua ya kumkejeli mgonjwa au mtu aliyeishiwa eti kafulia!
Ieleweke kuwa kinachoua sanaa ya ucheshi ni pamoja na kukosa ubunifu, dharau (mfano unaposema sisi tunalipwa nyinyi mnacheka), uongozi usio na malengo, kutokujua watazamaji wanataka nini, na kulewa umaarufu.

Baadhi ya wasomaji wamewahi kunipigia simu na wengine kuniandikia ujumbe mfupi kunitaka nizungumzie suala la hizi zinazoitwa komedi, vimbwanga, futuhi na mengine mengi, na wengine wakashauri kuwa ni bora turudi kwenye visa na vituko vya kina Ndumilakuwili, Kipepe, Lodi Lofa, Madenge, Pimbi, Kifimbo cheza, Sokomoko na wengineo.

Kila jamii ina utamaduni wa kipekee sana wa kuchekesha. Bahati mbaya Watanzania tumeathiriwa na mifano ya nje. Vijana wa Tanzania wameshindwa kuelewa kwamba tunatazama filamu za nje kwa ajili ya kuangalia wenzetu wanafanyaje kazi zao lakini si kuiga kwani si mwalimu mzuri kwetu.

Feb 8, 2011

Steps na Pilipili Entertainment kwenda kimataifa

 Nembo ya filamu ya nchi za Caribbean

Nembo ya Tamasha la Filamu Zanzibar

Poster ya filamu ya Deception

Kampuni ya usambazaji wa filamu ya Steps Entertainment na ile ya utengenezaji filamu ya Pilipili Entertainment ziko mbioni kupata soko la kimataifa kutokana na filamu zao kunadiwa katika tamasha la kimataifa la Fair International Film Festival sambamba na Iran Film Market.

Taarifa za kampuni hizi zimetolewa na Meneja wa Zanzibar International Film Festival (ZIFF), Daniel Nyarusi kutoka Iran kuwa watatumia filamu za kampuni hizo kupata soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa Ziff, wanajaribu kupata wasambazaji, wazaalishaji na wawekezaji wa filamu duniani, ambao wangependa kununua, kusambaza, kutengeneza au kufanya kazi ya pamoja na kiwanda cha filamu hapa nchini.

Feb 2, 2011

Pamoja na changamoto, soko la filamu litakua na kudumu! KULIKONI, FEB 4, 2011

 Said wa Ngamba, mmoja wa waigizaji nguli
katika tasnia ya filamu Tanzania

 Baadhi ya waigizaji wakiwa kwenye kikao cha wadau wa filamu

*Wauzaji wa filamu wanapaswa kushirikiana na 
  makampuni yenye mitandao nchi nzima
*Mafunzo juu ya maarifa pia yapewe kipaumbele

USIKU wa Jumatatu wiki hii sikupata usingizi kabisa, nilijiwa na mawazo yaliyoshindikana kufutika akilini mwangu, mawazo ambayo yameendelea kunitesa hadi niandikapo makala hii, kuwa kuna nguvu kubwa inayotambaa mikononi mwa wauzaji wa filamu nchini... Kubwa sana.

Kitendo kinachofanywa na wauzaji kuwa na umuazi wa mwisho kama wauze kazi au la, na hakuna njia mbadala kinazidi kuwatesa watayarishaji wengi wa filamu hapa nchini.

Mwisho wa wiki iliyopita kulikuwa na kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania wakilalamikia kitendo cha msambazaji mmoja mkubwa kuwadhibiti wasambazaji wadogo kwa kujipangia bei ambayo wasambazaji wengine hawataweza kufanya biashara.

Viongozi wa shirikisho walitaka iwepo sheria ya udhibiti itakayopanga kiwango maalum kitakachotumiwa na wasambazaji wote ili kuleta uwiano mzuri na tija katika biashara, lakini walijikuta wakisalitiwa na wasanii na watengeneza filamu wenzao kudhoofisha hoja zao.

Wakati viongozi wa shirikisho wakiwa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wenzao (wenye mkataba mnono na msambazaji anayelalamikiwa) waliwahi ofisini kwa Waziri wa wizara husika kulalamika kuwa kikundi cha watu wachache wenye mpango wa kuivuruga tasnia ya filamu wamepeleka madai yasiyo na maana kwa mkuu wa mkoa!

Kilichofanywa hapa kimetokana na kutumia nguvu ya pesa na hakina tofauti na hadithi ya mpini (mti) unaowekwa kwenye shoka na kutumiwa kuimaliza miti mingine.

Ndiyo maana nahisi kuwa shirikisho la filamu Tanzania lazima lisaidiwe kufanikiwa katika hili, bila kujali. Ni lazima lifanikiwe kwenye hili kwa mustakabali wa tasnia ya filamu nchini.

Tuna waongozaji filamu wenye uwezo mkubwa wa kuihabarisha jamii kupitia tasnia ya filamu katika 'angle' mbalimbali, ingawa inakuwa vigumu kwao kutengeneza sinema kwa ufanisi na kwa kiwango kizuri kutokana na mparaganyiko uliomo ndani ya tasnia hii.

Leo nitajaribu kubainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili tasnia hii, na kwa nini ni muhimu kwa wasanii kupewa muongozo (script) wiki chache kabla ya upigaji picha.

Nikiwa mmoja wa wanaharakati wa sanaa ya filamu, naziangalia changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya filamu hapa nchini wakati huu, kubwa ikiwa ni masoko ya sinema (hasa kwa wasambazaji wadogo). Hii ni kwa sababu soko letu si kubwa na halijasambaa sehemu kubwa japo kuenea Afrika Mashariki.

Wengi wa wasambazaji walio katika soko la sinema la nchi hii, hufanya biashara ama wakiwa Dar es Salaam au Mwanza, bila kupanua mtandao wa masoko yao sehemu nyingine.

Changamoto ya pili ni suala la uharamia wa kazi za sanaa ambalo ni dhahiri imekuwa tatizo, si tu kwa watengenezaji wa filamu, lakini hata kwa waandishi pia, kwa hiyo, kwa maoni yangu, ufumbuzi wa tatizo ni lazima wauzaji wa kazi za sanaa wafikirie kuanzisha ushirikiano tofauti na ilivyo sasa. Hapa nawakusudia wasambazaji wadogo.

Wasambazaji wa filamu wanatakiwa kutafuta namna ya kupata mafunzo juu ya maarifa yao kuhusu masoko. Masoko si kuuza tu bidhaa bali pia inahusu ushirikiano. Inahusu namna ya kupanua mtandao wa mtu mmoja mmoja au kundi.

Kama msambazaji ana duka Mwanza, na katika miaka miwili, msambazaji huyo hajaweza kupanuka zaidi, basi ni bora akafanya mpango wa kutafuta washirika wengine wa kibiashara au chombo/mashirika mengine kwa ajili ya usambazaji wa sinema zake.

Kuna vyombo/mashirika ambayo yamefanikiwa kuwa na mitandao karibu nchi nzima, wasambazaji/wauzaji wa filamu wanaweza tu kushirikiana na mashirika hayo kwa ajili ya usambazaji wa sinema katika maeneo mengi nchini.

Hivyo kama mtandao wa usambazaji wa filamu wa msambazaji fulani utakua na kupanuka zaidi, basi faida katika uwekezaji kwa waandaaji filamu pia itakuwa kubwa na kuwafanya kuwa na pesa zaidi zitakazowawezesha kufanya utafiti, na watakuwa na uwezo wa kuwalipa wasanii wao vizuri kuliko ilivyo hivi sasa.

Kwa sasa, asilimia ya watu wanaofaidika na uzalishaji wa filamu hapa nchini iko chini ya asilimia 15. Hawa ni muigizaji mkuu, Muongozaji mkuu, Mpigapicha, na watu wengine wachache, lakini watu wengine waliobaki katika tasnia hii hasa kwenye uzalishaji hawapati kabisa kile wanachostahili kupata. Kwa mfano, kama kuna watu 30 katika eneo la upigaji picha (location), ni watu wachache mno wasiozidi 5 ndiyo watakaopata malipo stahiki kutokana na kazi hiyo ya uzalishaji.

Hivyo, kama kutakuwepo soko pana zaidi kwa sinema, walio wengi katika eneo hili la uzalishaji wataweza kupata mishahara/posho nzuri itakayowawezesha kuishi vizuri.

Changamoto nyingine ambayo lazima tuikubali ni kuhusu lawama kwamba sinema nyingi mno zinazotengenezwa nchini zimezama zaidi kwenye mapenzi, mauaji, ukahaba na uchawi. Nimewahi kuulizwa na wasomaji kwa nini inakuwa hivyo? Au hatuna hadithi nyingine ambazo tunaweza kuzitumia?
Ikumbukwe kuwa utengenezaji wa sinema ni jambo linalohitaji sana mgawanyo wa kazi (division of labour). Kuna waongozaji, waigizaji, waandishi wa miswaada (scriptwriters) na kadhalika, lakini msingi mkuu wa sinema yoyote ni mwongozo (script). Hapa haijalishi kabisa uzuri wa kisa (plot), kama hadithi haiko katika mpangilio mzuri, basi itakuwa ni kazi bure.

Hakuna kisa kinachoweza kuifanya sinema ipendeze bila kuwepo 'storyline' nzuri. Hii inamaanisha kwamba endapo waandishi wa miongozo watalipwa vizuri, watakuwa na uwezo wa kufanya utafiti wa kina kabla hawajakimbilia kuandika muongozo.

Inaweza hata kuwachukua zaidi ya mwaka mmoja kufanya utafiti wa hadithi wanazohitaji kuziandika, kwa sababu watazama kwenye kina cha habari, kujua ni nini hasa kinachoendelea katika hali halisi ya maisha ya jamii kuhusiana na hadithi wanayohitaji kuiandika.

Wataweza kufanya mahojiano na watu wengi kuhusiana na hadithi waliyoikusudia. Utengenezaji wa sinema pia hufafanuliwa kwa lugha ya kigeni kama 'make-believe world', hii ni kwa sababu hadithi yoyote iwavyo, ni lazima iakisi maisha halisi ya jamii. Kwa hiyo, waandishi wenye ujuzi ni muhimu sana kwa ajili ya kuiokoa sekta yetu ya filamu.
Leo hii, kila mtu anaamini kuwa anaweza kuandika hadithi nzuri, na kinachoumiza zaidi ni ule ukweli kwamba waandishi hawa hawajawahi kuhudhuria japo warsha juu ya uandishi au kujiendeleza kwa kozi yoyote ya uandishi wa skripti.

Kwa maana hiyo, hii ndiyo imekuwa sababu ya haya yote kutokea katika mtizamo wa aina moja, wakati kuna mitazamo elfu moja na moja ambayo mada zinaweza kuwasilishwa. Hivyo, hadi tutakapokuwa na waandishi wazuri na waongozaji wazuri, suala la kutengeneza sinema ya mada fulani kutoka 'angle' moja tena na tena litaendelea. Hii ni changamoto nyingine ya kutothamini kujiendeleza kielimu.

Kwa nini nashauri kuwapatia wasanii skript wiki chache kabla ya upigaji picha? Kufanya hivi ni muhimu kwa sababu humpa muongozaji muda zaidi wa kuifanyia kazi hadithi.

Kile kinachowasilishwa katika hadithi kinaweza kuwa hakijawahi kutokea kabisa. Hivyo, kwa sababu ya hili, wasanii wanahitaji kupewa muda wa kuisoma hadithi, kuitafakari kwa kina ili kuielewa, na ikiwezekana, kufanya utafiti wao wenyewe juu ya nini wanataka kuwasilisha, hivyo kwa wakati wapokwenda kwenye eneo la upigaji picha (on set), watakuwa wamewiva kihisia kulingana na mahitaji ya hadithi, na kuwa na uwezo wa kutoa tafsiri halisi ya wajibu wao wanapocheza.

Hii ni muhimu kwa sababu miongoni mwa watazamaji, kuna watu ambao wamekuwa na uzoefu mkubwa kuliko kile wasanii wanachokiwasilisha, na uwasilishaji wowote usio sahihi kwa uzoefu huu, watakuwa wameiangusha sinema na kupelekea mauzo kushuka.

Kwa mfano, msanii anapowasilisha katika nafasi ya udaktari, mpelelezi au mwanasheria ni lazima apate muda wa kutosha kufanya utafiti jinsi gani hawa wataalamu wanavyofanya au kutenda katika maisha yao halisi, endapo atawasilisha kitu kingine tofauti na hali halisi itakuwa ni janga kamili.

Tusisahau kwamba kuna madaktari, wapelelezi na wanasheria ambao pia wanaangalia sinema hizi, hivyo uwasilishaji wowote usio sahihi kuhusu majukumu yanayowasilishwa na wasanii, utawafanya wataalam hawa kupoteza imani au hamu ya kufuatilia kazi hizi.

Hivyo, nashauri kuwapa wasanii skript mapema ili wawe na muda mwingi wa kufanya utafiti kuhusu majukumu yao kwenye sinema. Pia uibuaji wa vipaji utasaidia pale ambapo wasanii maaruf wanaodhani kuwa wamefika na hawana kabisa muda wa kusoma skripti.

Alamsiki