Bayport

Bayport

fofam

fofam

imetosha

imetosha

Ads

Ads

Jan 1, 2010

Nawatakia wote Heri ya Mwaka Mpya, 2010Naitwa Bishop John Hiluka (nilizaliwa siku ya Alhamisi, Machi 26, 1970, siku tatu kabla ya Sikukuu ya Pasaka, saa kumi na moja alfajiri), ni Mtanzania Muongozaji wa Filamu, Mwandishi wa Miswada ya Filamu (Scriptwriter), Mchoraji wa picha za hadithi (Comic Artist), Tabibu (Medical Personnel), Mtaalam wa sauti (Sound Expert) na Mtafiti ambaye nina uzoefu mkubwa katika ubunifu na uandishi kwa ajili ya sinema na uongozaji wa sinema. Nimeshiriki kama Mshauri, Muongozaji, Mwandishi wa Miswada ya Filamu, Meneja Uzalishaji, Mbunifu, Mtaalamu wa sauti nk katika miradi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 10.

Bishop J. Hiluka

Maisha ya awali

Nlizaliwa katika Hospitali ya Wamisheni ya Ndala iliyopo katika Wilaya ya Nzega, Tabora, kutoka kwenye familia ya baba Mngoni na mama Mnyamwezi. Mama yangu, Catherine Kimwaga (alizaliwa 15 Februari 1945 na kufariki ghafla tarehe 20 Desemba 2004 akiwa safarini akitokea Dar es Salaam kuelekea Tabora) alikuwa mfanyakazi wa Hospitali wilayani Nzega. Baba yangu Mzee Alex M. Hiluka, pia alikuwa tabibu kabla hajajikita kusomea masuala ya.lishe na kuwa Afisa Mtaalam wa Lishe na Mkuu wa Idara ya Lishe, Makao Makuu katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, jijini Dar es Salaam.
 

Ni mimi Bishop J. Hiluka, hapa nikiwa na miezi mitatu tu

Baba yangu alitengana na mama yangu baada ya kuondoka wilayani Nzega alikokutana na mama na kuhamia jijini Dar es Salaam kama Afisa Mtaalamu wa Lishe katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hata kabla sijazaliwa, Mama alibaki Wilayani Nzega, baada ya miezi michache nikazaliwa. Muda mwingi wa utoto wangu niliutumia kuishi na mama ambaye alikuwa akihamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine kutokana na kazi yake, lakini san asana ikiwa ni katika wilaya za Nzega na Kahama, na mara chache nilimtembelea baba yangu jijini Dar es Salaam. Katika maisha yangu ya ujana, nilitaka sana kufanya "adventures" katika filamu, ingawa kiukweli nilipenda sana kufanya mojawapo ya kazi mbili: Upelelezi (Usalama wa Taifa) au Uandishi wa habari za uchunguzi (Investigative journalism). Nilipenda kazi hizi ambazo pamoja na upeo wangu kuwa mdogo niliziona zikishabihiana kwa mambo mengi ikiwemo uchunguzi wa kina, utafiti na umakini katika kufuatilia taarifa. Nilisamehe chakula hata nilipokuwa na njaa endapo mtu angeanza kusimulia hadithi au kisa cha aina yoyote. Nilijenga taswira ya kitu kilichosimuliwa akilini mwangu na kukiona kama vile naangalia sinema kitu ambacho kilinifanya nianze kupenda kujisomea na kuandika visa mbalimbali tangu nikiwa mdogo. Hadi sasa mfumo wa maisha yangu umetawaliwa na mambo haya; uandishi na uchunguzi, nikilala, nikitembea, na chochote nifanyacho huwa nafikiria kuandika/kufuatilia taarifa tu. Uandishi na utafutaji wa taarifa imekuwa ni sehemu ya maisha yangu. 

Mwaka 1978, katika umri wa miaka 8, nilianza elimu yangu ya msingi katika shule ya msingi Itobo, wilayani Nzega na baada ya miezi michache mama yangu alihamishiwa Igusule ambako niliendelea na masomo yangu ya shule ya msingi. Mwaka 1982 nilihamia katika Shule ya Msingi Ngogwa, wilayani Kahama na mwaka mmoja baadaye nilirudi tena katika Shule ya Msingi Igusule, wilayani Nzega. Nilimaliza elimu yangu ya msingi mwaka 1984, katika umri wa miaka 14, kisha nikaendelea na masomo zaidi. 

Ingawa nilikuwa na akili nyingi (sijisifu lakini ndiyo ukweli wenyewe) nilijikuta nikishindwa kuendelea na masomo kutokana na matatizo makubwa ya kifamilia yaliyokuwa nje ya uwezo wangu na uwezo na mzazi wangu aliyepaswa kunisomesha, lakini kwa kuwa nilikuwa na ndoto nilizojiwekea nililazimika kujiendeleza kimasomo na hatimaye nikafaulu vizuri katika masomo ya sayansi na kujiunga na mafunzo ya Utabibu (Clinical Course). Kwa kuwa niliipenda sana sanaa, mwaka 1988, katika umri wa miaka 18, nilijiunga na kundi laa sanaa za maonyesho la Mwasama Acrobatic Group wakati nikiwa bado katika masomo yangu, na hiyo kwangu ilikuwa ni hatua moja muhimu katika kutimiza ndoto zangu. Septemba 1 1990, katika umri wa miaka 20, nilijiunga na Shule ya Tiba kwa ajili ya masomo ya Stashahada katika Tiba na kuhitimu mwaka 1993, katika umri wa miaka 23. 

Upande wa dini, mimi si muumini wa imani za kiroho, kama mtoto, nilikuwa na wakati mgumu sana kukubali dini ambayo familia yangu iliifuata. Si kitu ninachopenda kukiri hadharani, lakini wakati nikiwa bado mdogo hadi kwenye ujana wangu, nilikuwa nikihudhuria sana kanisani kila Jumapili, mwaka 1980 (kama kumbukumbu zangu ziko sahihi), nilipata Komunio ya Kwanza, na baadaye mwaka 1983 nilipata Sakramenti ya Kipaimara katika Kigango cha Igusule, Jimbo Katoliki la Kahama. Mama yangu na babu yangu upande wa mama walitaka nisome kwa bidii na siku moja lazima niwe padri. Kazi rasmi katika sanaa ilianza niliporejea jijini Dar es Salaam kutoka Francistown nchini Botswana mwaka 1998 nilipoamua kuachana na kazi utabibu (Clinician) na kuingia kwenye sanaa. 

Kitaaluma mimi ni tabibu (Medical Personnel) niliyefuzu na kufanya kazi ya kutibu wagonjwa kwa takriban miaka miwili huko Morogoro. Baadaye nikaingia kwenye mkumbo unaowakumba wataalam wengi wa kiTanzania kukimbilia nje ya nchi kufanya kazi. Nilikwenda Gaborone, Botswana na baadaye nikahamia katika mji mwingine wa Francistown. Huko sikudumu na taaluma ya tiba, niliiacha nikaingia kwenye sanaa.

Wakati nikiwa Morogoro niliwahi kupata bahati ya kukutana na gwiji la uandishi wa riyawa nchini Tanzania na mmoja wa waandishi wanaoheshimika sana hadi leo, huyu alikuwa Eddie Ganzel, ambaye kwa sasa ni marehemu. Nilitambulishwa kwake na rafiki yangu aliyekuwa jamaa yake wa karibu.

Eddie Ganzel ndiye mwalimu wangu wa kwanza katika uandishi, alinifundisha misingi muhimu ya uandishi. Siku ya kwanza tulipokutana nilijua kuwa nimepata nafasi adimu na sikutakiwa kuzembea, nikamtupia swali; “Ni ushauri gani unaweza kunipa ili niwe mwandishi mzuri?” Eddie Ganzel aliyekuwa akiandika riwaya wakato huo, aliinua uso huku akiivua miwani yake na kunitazama kwa muda kama vile anatafuta jibu, kisha akaniambia; “Fanya mambo matatu: Jifunze kuandika, jifunze kuandika, ifunze kuandika.”

Sikuwa nimemwelewa kabisa! Ilinichukua miaka mitatu kuelewa alichomaanisha, hasa baada ya kupata mafunzo ya awali ya uandishi na kujikita katika uandishi. Wakati nikirejea nchini tayari nilikuwa nimepata mafunzo ya awali ya uandishi wa miswada ya filamu, lakini sikuweza kufanya kazi za filamu kwa kuwa wakati huo sekta ya filamu nchini ilikuwa bado ipo gizani. Kwa hiyo nilijiunga na kampuni ya Gaba Africa, wachapishaji wa jarida maarufu la cartoon la ‘Kingo’. Hapo nilianza kama msanifu wa hadithi za michoro (Comic stories), kipaji nilichokuwa nacho tangu nikiwa shule ya msingi.

Baadaye nilijiendeleza katika kuandika hadithi na makala baada ya kupata hamasa kutoka kwa James Gayo, mchora katuni (cartoonist) maarufu na mwanzilishi wa gazeti la Kingo. Ilikuwa ni wakati huo (1998) nilipokutana na wakongwe wa masuala ya filamu; Julius Mhilu (aliyekuwa katika kundi la maigizo la Chuo Kikuu cha dare s Salaam, Idara ya sanaa) na Richard Ndunguru, (kwa sasa mhadhiri wa sanaa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam). Mhilu ndiye aliyefanya ndoto yangu kuwa kweli kwa kunisaidia kwenye mambo mengi ili kutimiza matakwa yangu. Ni katika wakati huo nilipoanza kukutana na magwiji wengine katika sanaa, na kupata hamu ya kujiendeleza zaidi ambapo nilichukua masomo ya uandishi wa kiuumbaji (Creative writing) INTEC College, Afrika Kusini.

Kazi za Sanaa

Kama nilivyosema, Julius Mhilu aliibua chachu baada ya kuniunganisha kwenye kazi moja iliyoandaliwa na Kituo cha Televisaheni cha China (CCTV) mwaka 1999 – 2000, wakati walipokuja kutengeneza sinema yao iitwayo “Africa Forever” mimi nilifanya kazi kama mmoja wa watendaji kwenye kazi hiyo. Baada ya kazi hii, nilianza kushiriki katika kazi mbalimbali za sanaa ya maigizo. Nilikuwa miongoni mwa waanzilishi wa kundi lililopata umaarufu mkubwa la michezo wa kuigiza la Nyota Academia 2000, kabla ya kuondoka tena nchini na kwenda Lilongwe, Malawi katikati ya 2001. Nilirudi Tanzania mwaka 2002.

Kuanzia mwaka 2003

Mwaka 2003 nilishiriki katika kazi mbalimbali za filamu kama “BIFU (2004)” iliyoandaliwa na Do Inc. kwa kushirikiana na 2 Eyes Production, Vichekesho vya “WANDANI (2003-4)” vilivyoandaliwa na Afrikan Image Production Ltd  na kuchaguliwa na MNET kwa ajili ya kurushwa kwenye Chaneli ya Africa Magic, “TUMAINI (2004)” iliyoandaliwa na Abantu Vision na kushinda Tuzo za UNICEF kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu la Nchi za Majahazi (ZIFF) na KIPUSA (2004) iliyoandaliwa na Trinity Inc. Na hii ilikuwa ni hatua muhimu sana katika kujihusisha na shughuli za filamu.

Uigizaji

Isisahaulike kuwa mimi pia nimewahi kuigiza, nathubutu kusema ni muigizaji mzuri. Nimeshaigiza katika sinema kadhaa kama mhusika wa ziada (kwa kuwa sipendi kujiingiza zaidi kwenye uigizaji), kwenye sinema kama NAOMI (2007-08) iliyoandaliwa na Studio KVS, na PESA (2007) iliyoandaliwa na Aminaah Studio.

Maisha binafsi

Maisha ya ndoa na watoto, mwaka 2000, nilimuoa Batoul Yahya, lakini tulitengana mwaka mmoja baadaye, kabla sijatimkia nchini Malawi. Mwaka 2003 nilijiingiza kwenye uhusiano na Winfrida Thomas, tuliyeishi nyumba moja Magomeni Mikumi, jijini Dar es Salaam, wakati huo akiishi na dada yake. Tulioana mwaka 2004 na tuna mtoto mmoja, Magdalena Hiluka, aliyezaliwa Oktoba 6, 2004.

Filamu nilizoshiriki

Ifuatayo ni orodha ya filamu nilizoshiriki katika nafasi mbalimbali:

  • Muigizaji: Naomi Film (2007-08) na Shekeli "PESA" - (2007)
  • Mwandishi wa Miswada ya filamu: You Must Pay (2009), Blackmail (2009), New Page (2009), From China With Love (2008), Naomi 1 (2007-08), The Pain (2007), Love is War (2007), My Heart (2007-08), Silence Killer (2007), The Trip (2007), Pesa (2007), Miss Bongo (2007), Jeraha la Ndoa (2007), Sandra (2005), Kipusa (2005), Vichekesho vya Wandani (2004)
  • Muongozaji wa filamu: Blackmail (2009), Naomi 1 (2007-8), Kipusa (2005)
  • Mshauri: Mtoto wa RPC (2007), Bifu (2004), Black Suit (2009), Tell Me (2008)
  • Meneja Uzalishaji: Pesa (2007), Tumaini (2005), Bifu (2004)
  • Mbunifu: Africa Forever (1999-2000)

Hivyo, nawatakia Heri ya Mwaka Mpya 2010 wasomaji wote wanaofuatilia blog hii, Mungu awabariki sana. Samahani kwa kuwa kimya kwa kipindi kirefu nitarudi hivi karibuni na kuwapatia mambo mapya.

Endeleeni kufuatilia habari za kina zinazohusu tasnia ya filamu na sanaa za Tanzania kwa ujumla kwenye blogu hii...

No comments: